Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WIPO yazungumzia nafasi ya teknolojia katika usafiri wa zama zijazo

Roboti ya Nono-Y ilikuwa mojawapo ya vivutio vya Maonesho ya Uvumbuzi ya Geneva ya 2012.
WIPO/Emmanuel Berrod
Roboti ya Nono-Y ilikuwa mojawapo ya vivutio vya Maonesho ya Uvumbuzi ya Geneva ya 2012.

WIPO yazungumzia nafasi ya teknolojia katika usafiri wa zama zijazo

Tabianchi na mazingira

Teksi za angani, ‘magari yanayojiendesha yenyewe, na roketi zinazoweza kutumika tena na tena, ni baadhi tu ya majawabu ya  usafiri wa siku zijazo ambazo wavumbuzi kote ulimwenguni wanajitahidi kutafuta kuwa uhalisia, wakati huu ambapo mwelekeo wa hakimiliki za injini zinazohitaji kuchoma mafuta ndio ziendeshe mashine ukiwa mashakani.

Hiyo ni kauli ya shirika la Umoja wa Mataifa la miliki bunifu (WIPO) iliyotolewa leo kupitia ripoti yake ya Mwelekeo wa Teknolojia kuhusu Mustakabali wa Usafiri.

Ripoti hiyo ikionesha ongezeko la maombi ya hakimiliki ya vifaa hivyo vya usafiri ikiwa ni mwanga wa kuvutia kuhusu mustakabali wa siku chache zijazo wa usafiri wenye uchafuzi mdogo wa mazingira, msongamano mdogo wa magari, na safari za anga hadi upande mwingine wa dunia – zikifanyika kwa muda wa saa chache tu.

“Uchambuzi wa hakimiliki unaonesha kuwa wavumbuzi wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa usafiri wa siku zijao unakuwa safi na bora zaidi kuliko wa leo,” imesema WIPO, ambayo imeeleza kuwa maombi ya hakimiliki  kwa majawabu ya usafiri wa siku zijazo yameongezeka kwa asilimia 700 katika miongo miwili iliyopita, kutoka uvumbuzi 15,000 mnamo 2003 hadi 120,000 mnamo 2023.

“Meli zinazojiendesha na bandari mahiri zinabadilisha usafiri wa baharini; magari ya umeme, treni za mwendo kasi na mifumo ya usimamizi wa trafiki mahiri zinaendesha mageuzi ya usafiri wa nchi kavu,” imesisitiza WIPO.

“Ndege zinazoweza kuruka na kutua wima zinatoa njia mpya za kusafiri angani, huku roketi zinazoweza kutumika tena na tena na teknolojia za satelaiti zikipanua uwezekano nje ya anga ya dunia.”

Kinachoendesha mwelekeo huu ni utambuzi kwamba sekta ya usafiri inachangia zaidi ya theluthi moja ya uzalishaji wa hewa ya kaboni au ukaa, duniani, jambo ambalo limehamasisha maendeleo ya teknolojia endelevu zinazopunguza athari za kimazingira za usafiri.

Hizi ni pamoja na kupitishwa kwa mifumo ya uendeshaji wa umeme, mabadiliko kuelekea vyanzo vya nishati vinavyoweza kurejeshwa na uendelezaji wa chaguzi za usafiri wa umma na wa pamoja.

Maendeleo ya kidijitali pia yanabadilisha sekta ya usafiri, WIPO inasisitiza, ikitaja kuongezeka kwa uendeshaji wa magari yanayojiendesha, “ambayo yanatarajiwa kuingiza mapato ya kati ya dola bilioni 300 hadi 400 kufikia 2035.”

Ukweli wa hakimiliki

Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa ,miliki bunifu inasaidia uvumbuzi wa aina hii wa mageuzi – kama vile malipo ya umeme bila waya kwa magari ya umeme – kwa kuhamasisha uwekezaji katika utafiti na maendeleo.

“Mashindano ni makali kwani kampuni zinashindania kupata madini adimu, huku akili mnemba (AI) pia ikichukua nafasi ya msingi,” WIPO inasema.

“Ripoti pia inaonesha ukuaji uliodumaa wa shughuli za hakimiliki kwa bidhaa za zamani kama vile injini zinazohitaji kuchoma mafuta kisukuku ziweze kuendesha mashine,  na mifumo mingine inayotegemea mafuta ya kisukuku” kama vile vifaa vya kusafisha hewa chafu kutoka kwenye gari, inasema WIPO.

Takwimu zake zinaonesha kuwa zaidi ya uvumbuzi milioni 1.1 wamebadilisha sekta ya usafiri tangu mwaka 2000, wakileta matarajio ya mbadala endelevu kwa mifumo inayotegemea mafuta ya kisukuku, kama vile seli za nishati mbadala, teksi za angani na meli za mizigo zinazojiendesha.

Nchi zinazoongoza kwenye mageuzi ya usafiri

Katika uongozi wa mageuzi haya ya usafiri ni China, Japani, Marekani, Korea Kusini na Ujerumani, ambazo zinawakilisha wavumbuzi wakuu wa dunia.

Hakimiliki za usafiri wa nchi kavu ndizo zinazoongoza duniani, zikiwa mara 3.5 zaidi ya zile za anga, baharini na angani kwa pamoja. Marekani, kwa upande wake, imewasilisha hati miliki nyingi zaidi kimataifa.

Sehemu kubwa zaidi ya ukuaji katika uwasilishaji wa hakimiliki inahusiana na mifumo endelevu ya uendeshaji – kama vile betri za magari ya umeme au seli za hidrojeni – ambazo zinawakilisha juhudi za kuhakikisha kuwa watu na bidhaa zinasafirishwa kwa njia “safi, rafiki zaidi kwa hali ya hewa”.

Wataalamu wanaochunguza majawabu ya usafiri wa siku zijazo wanasema kuwa akili mnemba au AI,  pia iko tayari kuchukua nafasi muhimu.

Wanataja kuongezeka kwa uendeshaji wa magari yanayojiendesha, ingawa miundombinu haijabadilika haraka vya kutosha kuruhusu magari hayo kuchukua nafasi kamili, ripoti ya WIPO inabainisha.

Sintofahamu kuhusu droni

Uhaba wa madini, wakati huo huo, utaamua iwapo dunia inaweza kupitisha magari ya umeme kwa kiwango kikubwa – magari ambayo mwandishi mwenza wa ripoti hiyo, Christopher Harrison, anasema huenda yasiwe suluhisho la miujiza kwa wamiliki binafsi.

“Kutumia madini haya adimu na yenye mipaka katika gari la umeme la matumizi binafsi ambalo linatumika kwa asilimia chache tu ya siku si matumizi bora ya rasilimali hizo,” amewaambia waandishi wa habari.

Katika sekta ya anga, droni zitaendelea kupaa juu

“Sipendi kutazama juu na kuona anga lililojaa droni zikileta pizza au jozi ya glovu nyumbani kwangu na kusababisha uchafuzi wa macho na kelele,” amesema Robert Garbett, mwanzilishi wa Drone Major Group, akinukuliwa kwenye ripoti ya WIPO.

“Iwapo usafirishaji unafanyika kwenye eneo la mbali ambalo ni gumu kufikiwa, watu watakuwa na uwezekano mkubwa wa kuukubali kama suluhisho lenye manufaa,” aliongeza, akitoa mfano wa usafirishaji wa dawa za dharura.

Kwa mujibu wa WIPO, ukuaji wa hakimiliki za usafiri nchini China umekuwa mkubwa kutokana na udhibiti wake wa hivi karibuni katika soko la magari ya umeme. Lakini mataifa mengine pia yamechangia kwa viwango vya juu vya uwasilishaji wa hati miliki, yakiwemo Sweden, Italia, India na Canada.