Nenda kwa yaliyomo

Taliban

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bendera nyeupe ya Taliban inaonyesha maneno ya shahada.
Wapiganaji wa Taliban, wakati wa kukera kwa 2021.
Polisi wa kidini wa Taliban wakimpiga mwanamke kwa sababu alivua burka hadharani, mnamo mwaka 2001.
Taliban akimuua mwanamke hadharani ambaye alikuwa ameshtakiwa kumuua mumewe, 1998. Mume huyo alikuwa mkali, na alikuwa akimpiga na kumfungia kwa miaka mitatu. [1]
Maeneo yaliyotawaliwa na Taliban mnamo 1996 (kijani).

Taliban ni harakati ya kidini, kisiasa na kijeshi ya Waislamu Wasunni iliyoanzishwa mnamo mwaka 1994 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan.

Ilitawala sehemu kubwa ya Afghanistan kati ya miaka 1996 na 2001 na baada ya kuondolewa madarakani na uvamizi wa Marekani mnamo 2001 iliendesha vita dhidi ya majeshi ya NATO pamoja na serikali mpya ya nchi. Mwaka 2021 ilishinda tena na kuchukua utawala wa Afghanistan.

Harakati hiyo ina wafuasi wengi pia kaskazini magharibi mwa Pakistan, hasa kati ya Wapashtuni.

Harakati ya Taliban ilianzishwa na Mullah Mohammed Omar mjini Kandahar kusini mwa Afghanistan pamoja na wanafunzi wa madrasa yake. Wanafunzi wa madrasa huitwa "taliban" kwa lugha ya Kiajemi. Shabaha yao ilikuwa kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia sharia ya Kiislamu. Wafuasi wake walishinda vikundi vingine nchini hadi kutwaa mji mkuu Kabul mnamo Septemba 1996 walipotangaza Emirati ya Kiislamu ya Afghanistan. Katika vita hiyo Taliban walipata msaada wa siri kutoka Pakistan.

Utawala wa 1996-2001

[hariri | hariri chanzo]

Taliban ilitawala Afghanistan kati ya 1996 na 2001. Wakati huo, viongozi wake walianzisha utawala uliofuata mafundisho juu ya jamii na aina ya sharia yenye kanuni kali kuliko nchi zote za Kiislamu[2] [3] [4] [5]. Ukosoaji mwingi wa Taliban ulitoka kwa wasomi muhimu wa Kiislamu. [6]

Walitumia kanuni za hadd katika urithi wa Kiislamu kama kukata mkono wa mwizi, kuua majambazi na kuua wazinzi kwa kuwapiga mawe. Adhabu hizo zilitolewa mara kwa mara bila daawa yaani bila kesi kuendesha kwa utaratibu.

Wanaume walipaswa kuingia msikitini wakiwa nje ya nyumba wakati wa sala.

Hasa namna yao ya kuwatendea wasichana na wanawake kwa jumla ilishtusha watu wengi duniani na pia wenyeji wengi katika miji ya nchi hiyo[7]:

  • Kuanzia umri wa miaka nane, wanawake hawakupaswa kuwasiliana na wanaume ambao si wa familia zao za moja kwa moja, au ambao hawajaolewa nao.
  • Hawakuruhusiwa kutoka kwenye nyumba wasipotembea pamoja na mume au ndugu wa familia yao.
  • Hawakupaswa kuonekana hadharani, bila kuvaa burka ambayo ni aina ya hijabu inayofunika mwili wote pamoja na kichwa na uso.
  • Hawakupaswa kuvaa viatu vya visigino virefu, ili wanaume wasiweze kuwasikia wakati wanatembea na kuamsha hisia za kingono.
  • Hawakuruhusiwa kusema kwa sauti kubwa hadharani, ili mgeni asiisikie. [8]
  • Madirisha yote kwenye ghorofa ya chini ya nyumba lazima yafungwe, ili wanawake wasionekane kwa wanaume wanapopita mtaani.
  • Kuchukua picha za wanawake au kutengeneza sinema zinazoonyesha wanawake kulikuwa marufuku. Hii inatumika pia kuhusu picha za wanawake kwenye majarida, vitabu, magazeti au kwenye maduka.
  • Wanawake hawakurusiwa kusishiriki mikutano ya hadhara.

Kwa jumla Taliban hawakutambua haki za binadamu kwa wanawake [9]. Shule za wasichana zilifungwa na wanawake hawakuruhusiwa kufanya kazi nje ya nyumba.

Kila aina ya sanaa, muziki na burudani zilipigwa marufuku kabisa chini ya utawala wao. Sanamu, uchoraji, picha, kamera, runinga, n.k. ziliharibiwa.[10]

Kaskazini mwa nchi vita iliendelea kwa sababu wananchi wa kule walipigana kwa silaha dhidi ya Taliban.

Kupinduliwa kwa Taliban 2001

[hariri | hariri chanzo]

Katika kipindi cha vita hiyo wapiganaji wenye itikadi kali kutoka Pakistan na Uarabuni walikuja kuwasaidia Taliban. Kati yao alikuwa pia Osama bin Laden aliyeunda kundi la Al-Qaeda nchini Afghanistan na kupanga mashambulio yake dhidi ya Marekani. Baada ya mashambulizi ya 11 Septemba 2001 Marekani ilidai Afghanistan imtolee bin Laden kwao lakini Taliban walikataa wakidai kuona kwanza ushahidi. Hatua hiyo ilifuatwa na uvamizi wa Marekani. Lengo la uvamizi huo lilikuwa kuondoa serikali ya Taliban, kuharibu al-Qaeda na kumkamata bin Laden. Hadi mwisho wa mwaka 2001, Taliban walishindwa kote nchini na kujificha mlimani au kukimbilia Pakistan.

Kurudi kwa Taliban

[hariri | hariri chanzo]

Ilhali Marekani pamoja na nchi nyingine za NATO zilikabidhi madaraka mengi kwa serikali mpya ya kizalendo, Taliban walianza upya kushambulia jeshi la wageni kutoka milima ya mpakani mwa Pakistan wakitumia mara nyingi mbinu za kigaidi na kusababisha vifo vingi kati ya raia[11].

Tangu mwaka 2010 walianza kudhibiti tena maeneo kadhaa ya vijijini katika milima ya nchi.

Katika miaka iliyofuata walizidi kushambulia jeshi la serikali ya Afghanistan na majeshi ya Marekani na nchi za NATO. Nchi za kigeni zilianza kupunguza idadi ya wanajeshi wao kwa tumaini kwamba serikali ya Afghanistan itaweza kujitetea.

Ushindi wa pili

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Februari 2020, serikali ya rais Donald Trump wa Marekani na Taliban walitia saini Mkataba wa Doha ambamo Marekani ingeondoa askari wote kutoka Afghanistan ifikapo 1 Mei 2021.[12] Rais mpya wa Marekani Joe Biden alitangaza kuwa kuondoka kwa nchi yake kutoka Afghanistan kutaanza Mei 1, 2021 na kumalizika mnamo Septemba 11, 2021, ambayo itakuwa miaka 20 haswa tangu mashambulio ya 11 Septemba. [13] Taliban waliahidi kutoshambulia wanajeshi wa Marekani lakini waliongeza mashambulio yao dhidi ya jeshi la serikali.

Baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa NATO na idadi kubwa ya Wamarekani, Taliban walianza kuvamia maeneo mengi ilhali nguvu ya jeshi la kitaifa liliporomoka. Mnamo 15 Agosti 2021, rais wa Afghanistan aliondoka nchini na Taliban waliteka Kabul.

Mwisho wa Agosti 2021, Taliban walidhibiti nchi yote isipokuwa jimbo la Panjshir, wapinzani walipojipanga chini ya aliyekuwa makamu wa rais Amrullah Saleh aliyetangaza kwamba amechukua nafasi ya rais kufuatana na katiba ya jamhuri.[14]

Baada ya kutwaa Kabul, wasemaji wa Taliban walitangaza kwamba wanataka kufuata siasa tofauti kiasi na ile ya zamani. Wasemaji walidai kwamba wataruhusu wanawake kufanya kazi na wasichana kusoma, kama wanakubali kuvaa hijabu. Walitangaza pia kwamba watasamehe wananchi wote waliowahi kupigana nao. Hata hivyo, Waafghanistan wengi walijaribu kukimbia nchi kwa njia mbalimbali.

  1. "ZARMINA'S STORY". www.rawa.org. Iliwekwa mnamo 2021-08-17.
  2. "Machtwechsel in Afghanistan - Das Frauenbild der Taliban". Schweizer Radio und Fernsehen (SRF) (kwa Kijerumani). 2021-08-17. Iliwekwa mnamo 2021-08-17.
  3. Mohammad, Azadah Raz. "As the Taliban returns, 20 years of progress for women looks set to disappear overnight". The Conversation (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2021-08-17.
  4. Narain, Vrinda. "The world must not look away as the Taliban sexually enslaves women and girls". The Conversation (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2021-08-17.
  5. Hoodfar, Homa. "Taliban 'has not changed,' say women facing subjugation in areas of Afghanistan under its extremist rule". The Conversation (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2021-08-17.
  6. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-08-19. Iliwekwa mnamo 2021-08-19.
  7. Michael Griffin (2001). Reaping the Whirlwind: The Taliban movement in Afghanistan. London: Pluto Press, pp6-11/159-165.
  8. "some of the restrictions imposed by Taliban in Afghanistan". www.rawa.org. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-07-03. Iliwekwa mnamo 2021-08-19.
  9. Dupree Hatch, Nancy. "Afghan Women under the Taliban" in Maley, William. Fundamentalism Reborn? Afghanistan and the Taliban. London: Hurst and Company, 2001, pp. 145–166.
  10. "The Death of the Buddhas of Bamiyan". Middle East Institute.
  11. https://www.fdd.org/analysis/2010/08/10/un-taliban-responsible-for-76-of-deaths-in-afghanistan/ UN: Taliban Responsible for 76% of Deaths in Afghanistan , August 10, 2010 , The Weekly Standard
  12. "Can the US exit Afghanistan?". Can the US exit Afghanistan?.
  13. CNN, Kevin Liptak. "Biden announces troops will leave Afghanistan by September 11: 'It's time to end America's longest war'". CNN. {{cite web}}: |author= has generic name (help)
  14. "Afghan Vice President Saleh Declares Himself Caretaker President; Reaches Out To Leaders for Support". News18 (kwa Kiingereza). 17 Agosti 2021. Iliwekwa mnamo 17 Agosti 2021.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)