Perfectae Caritatis
Siku ileile (28-12-1965) ambayo Mtaguso wa pili wa Vatikano ulitoa hati kuhusu uchungaji wa maaskofu ilitolewa hii nyingine kuhusu kurekebisha upya maisha ya kitawa, nayo pia msingi wake ni hati Lumen Gentium juu ya Kanisa ambamo watawa wana nafasi yao (sura ya sita).
Hati ilitolewa na Papa Paulo VI baada ya kupata kura 2321 dhidi ya 4 tu kati ya washiriki wa mtaguso huo.
Misingi ya urekebisho
[hariri | hariri chanzo]Mtaguso ulitaja marekebisho makuu tu ya kufanywa, ukimuachia papa ayatungie sheria hapo baadaye. Hasa ulisisitiza hali mpya ya utawa inayotakiwa kutokana na mambo matano: kushika Injili kama kanuni kuu, kufuata kiaminifu karama ya mwanzilishi na mapokeo bora ya shirika, kujihusisha na maisha na malengo yote ya Kanisa, kupima hali na mazingira ya watu wa leo, kuweka mbele maisha ya Kiroho kuliko mipango mingine. Ili kuzingatia hayo yote, sheria za watawa ziliagizwa zirekebishwe kwa kuwahusisha wanashirika wote.
Yanayohusu watawa wote
[hariri | hariri chanzo]Kabla ya kueleza juu ya aina mbalimbali za utawa, hati hiyo inasisitiza mambo kadhaa yaliyo sawa kwa zote: kushika mashauri ya Kiinjili, kujikatalia malimwengu, kuwekwa wakfu kwa Mungu juu ya msingi wa ubatizo, kulitumikia Kanisa, kutekeleza maadili, kumfuata Yesu Kristo kwa bidii kama jambo pekee la lazima, kuunganisha sala hasa na moyo wa kitume. Nafasi ya kwanza inayo maisha ya Kiroho yaliyo chemchemi ya upendo unaohuisha hata utekelezaji wa mashauri ya Kiinjili. Watawa katika kulisha maisha ya sala wazingatie kila siku Maandiko matakatifu halafu liturujia.
Aina za utawa
[hariri | hariri chanzo]Katika kutofautisha aina za utawa, kwanza yanatajwa mashirika yanayoshughulikia sala tu katika upweke na kimya; baadaye yanatajwa mashirika yale mengi yaliyoanzishwa waitimize huduma maalumu kwa niaba ya Kanisa na kama sehemu ya maisha yao ya kitawa; mwishoni yanatajwa mashirika yanayotakiwa kuunganisha kiaminifu ratiba ya sala na taratibu nyingine za kijumuia pamoja na utume fulani. Halafu hati inaongelea maisha ya kitawa ya mabradha na masista, ikisisitiza kuwa ni muhimu yalivyo, bila ya kuhitaji yakamilishwe na daraja takatifu. Vilevile inasisitiza sura ya mashirika ya kilimwengu yanayopaswa kutafuta utakatifu kwa kuishi katika mazingira ya watu wa kawaida: kwa ajili hiyo yanahitajika malezi bora.
Mashauri ya Kiinjili
[hariri | hariri chanzo]Baadaye hati inarudi kufafanua mambo yanayowahusu watawa wowote, hasa mashauri makuu matatu ya Kiinjili, ikitanguliza useja kwa kuwa ndio msingi hasa wa kubainisha waliowekwa wakfu kwa Mungu na kwa ufalme wake kwa namna ya pekee. Hati inaonyesha ubora wa useja na njia za kuushika sawasawa baada ya jaribio la kutosha. Halafu inasisitiza ufukara kama ushahidi unaothaminiwa sana siku hizi: basi, usiwe wa kiroho tu au wa binafsi tu, bali uonekane wazi katika maisha ya jumuia pia. Kuhusu utiifu umesisitizwa ukuu wa sadaka hiyo ambayo mtawa anaungana kwa hakika na matakwa ya Mungu kwa mfano wa Yesu. Pamoja na hayo ajitahidi kutoa mchango wake na kuwajibika chini ya viongozi kama mtu aliyekomaa. Upande wao viongozi wasitawale kwa mabavu bali waonyeshe upendo wa Mungu kwa mtawa, wakimheshimu na kumsikiliza na kumuachia nafasi ingawa wana haki na wajibu wa kumuagiza la kufanya. Pia mikutano na halmashauri vishiriki katika uongozi.
Maisha ya kijumuia
[hariri | hariri chanzo]Sifa nyingine ya mashirika ya kitawa ni maisha ya pamoja ambayo yamesisitizwa upya kwa kutia maanani misingi yake na utekelezaji wa upendo kamili katika ushirika wa kidugu. Kwa lengo hilo tunakuta himizo la kufuta matabaka kati ya masista na la kushirikisha zaidi mabradha katika maisha ya jumuia, pamoja na kibali cha kuleta usawa kati ya wanashirika makleri na walei.
Ugo na nguo za kitawa
[hariri | hariri chanzo]Katika kulinda utawa toka zamani unatumika ugo, ambao kwa baadhi ya watawa wa kike unafuata sheria za papa. Hati hii inadai hizo zirekebishwe, halafu zisibane wale wanaofanya utume fulani. Kinga nyingine ya watawa ni nguo maalumu. Kwa mara ya kwanza katika historia mtaguso mkuu uliongelea suala hilo na kulitia maanani kama alama ya kuwekwa wakfu, pamoja na kuagiza baadhi zibadilishwe.
Malezi
[hariri | hariri chanzo]Upande wa malezi hati hii imeyasisitiza sana kama msingi wa urekebisho, ikikataza watawa wasitumwe kufanya shughuli mara baada ya unovisi, bali waendelee kuundwa katika nyumba maalumu. Halafu malezi yaendelee maisha yote kwa ushirikiano wa watawa na viongozi wao, ambao wajitahidi hasa kuandaa walezi wa kufaa.
Kuanzisha, kuunganisha na kufuta mashirika
[hariri | hariri chanzo]Zinafuata taratibu kuhusu kuunda mashirika mapya, halafu kuhusu kueneza aina mbalimbali za utawa katika Makanisa machanga kwa kuzingatia utambuzi na utamadunisho. Mashirika yaendelee kutimiza shughuli zake maalumu kulingana na karama na nyakati pamoja na kustawisha moyo wa kimisionari. Yale yasiyostawi yakatazwe yasipokee tena wanovisi au yaunganishwe na lingine la kufanana nayo. Tofauti na muungano, mtaguso umependekeza pia shirikisho la monasteri au mashirika ya familia moja ya kiroho, vyama vya mashirika yenye kazi ileile, mabaraza ya wakuu wa mashirika yote ya nchi au jimbo fulani ili kurahisisha ushirikiano kati ya watawa, tena kati yao na maaskofu.
Miito
[hariri | hariri chanzo]Suala la mwisho ni namna ya kupata miito ya kitawa: hiyo ni kazi ya Kanisa lote, kuanzia mapadri, wazazi na walezi. Mashirika yenyewe yanaweza kujitafutia miito kwa kufuata taratibu za Kanisa, lakini njia bora ni kutoa mfano mzuri. Hatimaye watawa wote wanahimizwa kuitikia upya wito wao.