Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki
Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki (vilevile: Biashara ya utumwa ya pembetatu au Biashara ya utumwa ya ng'ambo ya Atlantiki) ni jina la kutaja aina ya biashara ambayo ilikuwa ikifanyika baina ya mabara matatu, yaani, Afrika (upande wa magharibi), Amerika na Ulaya (hasa katika pande za magharibi mwa Ulaya).
Biashara ilihusisha hasa wafanyabiashara kutoka Ulaya ambao walikuja na bidhaa za viwandani na kuvibadilisha na [[watumwa] na vitu vya thamani kubwa barani Afrika kama vile dhahabu, almasi, fedha na kadhalika ambapo wao walichukua watumwa na bidhaa nyingine na kwenda nazo Amerika.
Wakiwa huko, watumwa walizalisha malighafi za kilimo na madini ambapo Wazungu walizichukua na kuzipeleka Ulaya kwa ajili ya kutengenezea bidhaa nyingine.
Watumwa waliochukuliwa Afrika walisafirishwa kwa njia ya meli kupitia Bahari ya Atlantiki hadi huko Amerika ambapo walitiwa utumwani katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Mahusiano ya biashara ya namna hiyo yameunda "Umbo la Pembetatu" ambalo likaja kujulikana kama "Biashara ya Pembetatu".
Historia
Kipindi
Biashara hii inaaminika ilianza mwishoni mwa karne ya 15 na kukua hadi mwishoni mwa karne ya 18 ambapo ilikomeshwa mazima.
Washiriki
Washiriki wakuu wa biashara hii walikuwa wanatoka Ulaya ambao hao ndio waliokuwa wanashikilia biashara hii. Wengine walikuwa wenyeji wa Kiafrika (Watemi) ambao walikuwa wanatoa watumwa kwa wafanyabishara Wazungu kwa kubadilishana nao bidhaa za viwandani. Kituo kikuu cha kuanzia shughuli hizi za Biashara ya Utumwa ya Pembetatu ilikuwa Ulaya na biashara pia ilimalizikia hukohuko Ulaya (kifupi: Biashara inaanza barani Ulaya na kumalizikia barani Ulaya).
Biashara zilizohusishwa
Kutoka Ulaya
Kutoka Ulaya, wafanyabishara walileta Afrika bidhaa za viwandani kama vile nguo, vinywaji, sigara, bunduki na unga wake, mapambo, vyombo vya kupikia na vinginevyo ambavyo vilibadilishana kwa watumwa na mali njema nyinginezo za Kiafrika.
Kutoka Afrika
Kutoka Afrika, wafanyabiashara wa Kizungu walibadilishana biashara zao na kuchukua watumwa na bidhaa nyingine za thamani kama vile dhahabu, pembe za ndovu, fedha, na ngozi za wanyama. Watumwa walichukuliwa hadi Amerika na India-za-Magharibi (Visiwa vya Karibi) ili kufanya kazi katika mashamba makubwa na migodi iliyoanzishwa na Wazungu.
Kutoka Amerika
Kutoka Amerika, Wazungu walichukua malighafi za kilimo kwa mfano pamba, mkonge, majani ya chai na tumbaku na madini kisha kwenda nayo Ulaya kwa ajili ya kuzalisha viwandani.
Sababu zilizopelekea kuibuka kwa Biashara ya Utumwa ya Pembetatu
Kuna sababu mbalimbali zilizochangia kuibuka na kukua kwa Biashara ya Utumwa ya Pembetatu - nazo ni kama ifuatavyo:
(a) Kuibuka kwa daraja la wafanyabiashara huko Ulaya
Kuibuka kwa wafanyabiashara barani Ulaya kwenye karne ya 15 kulipelekea hitaji la mtaji mkubwa kwa ajili ya ukuzaji wa viwanda. Hili nalo lilipelekea kukua kwa biashara hii.
(b) Kugunduliwa kwa Amerika (Dunia Mpya)
Kugunduliwa kwa Amerika na Christopher Columbus mnamo 1492 kuliandaa kukua kwa Biashara ya Utumwa ya Pembetatu.
(c) Kuanzishwa kwa mashamba makubwa na migodi barani Amerika
Baada ya kugunduliwa Amerika, Wazungu walianzisha mashamba makubwa ya mazao aina mbalimbali kama vile pamba na tumbaku huko Magharibi mwa Indi. Hili lilihitaji wafanyakazi, hivyo basi lilipelekea kukua kwa biashara.
(d) Kushindwa kufanya kazi kwa Wahindi Wekundu katika mashamba makubwa
Awali, Wazungu waliwatumia wenyeji wa Amerika (Wahindi Wekundu) katika mashamba yao kama wafanyakazi. Lakini watu hawa walishindwa kufanya kazi kikamilifu jinsi Wazungu walivyotarajia. Hilo liliwafanya Wazungu waje Afrika kutafuta wafanyajikazi na hivyo basi biashara ikakua.
(e) Ukuaji wa teknolojia ya meli
Kukua kwa teknolojia ya meli (utengenezaji wa meli na mwongozo wa kidira) ulirahisisha usafirishaji baina ya Afrika, Amerika, na Ulaya. Kwa mfumo huu, ukuaji wa biashara ukawa hauepukiki tena.
(f) Mahali/nafasi ya kijiografia ya mabara matatu
Amerika, Afrika na Ulaya zimekaribiana mno. Hili nalo lilirahisisha ukuaji wa biashara.
(g) Upatikanaji wa watumwa katika Afrika Magharibi
Watumwa na vitu vingine vya thamani kama vile pembe za ndovu, dhahabu na almasi vilipatikana kwa wingi Afrika Magharibi. Hili lilipelekea ukuaji wa biashara kuwa hauepukiki.
(h) Nafasi ya viongozi wenyeji wa Afrika Magharibi
Huko Afrika Magharibi, baadhi ya viongozi walishirikiana na Wazungu kinaganaga katika kuratibu Biashara ya Pembetatu hasa kwa kukusanya watumwa na kuwasaidia wafanyabiashara wa Kizungu kupanga mikakati ya kibiashara na utelekezaji wake huko Afrika Magharibi. Kati ya hao viongozi alikuwemo Mfalme Agaja, Alfin Abipa, Alfin Ojago, na Alafin Ojig. Hili nalo lilichangia ukuaji wa biashara ya Pembetatu.
Matokeo/athari za Biashara ya Pembetatu katika Afrika
Baadhi ya matokeo ya biashara ya Pembetatu hasa huko Afrika Magharibi yalikuwa kama hivi:
Kulipelekea kupungua idadi ya watu - walienda utumwani
Waafrika wengi walichukuliwa kama watumwa na kupelekwa Amerika ili wakafanyaje kazi katika mashamba na migodi ya Wazungu. Hili lilipunguza idadi ya Waafrika hasa Afrika Magharibi.
Kulipelekea ukame na njaa kutokana na uzalishaji hafifu
Biashara ilipelekea kuleta ukame na njaa kwa sababu uzalishaji ulisimama hasa kwa kupoteza nguvukazi ya Afrika. Waliokuwa wanachukuliwa utumwa ni wale wenye miili yenye uwezo tu na si watoto wala watu wazima.
Ilipelekea familia kutengana
Biashara ya Pembetatu ilichochea mno utenganisho wa familia hasa kwa kufuatia kuchukua Waafrika kama watumwa na kuwapeleka Amerika na Indi-za-Magharibi.
Ilipelekea kuanguka kwa Biashara ya Ng'ambo ya Sahara
Biashara ilichangia mazima kuanguka kwa Biashara ya Ng'ambo ya Sahara. Mwishoni mwa karne ya 15], Biashara ya Ng'ambo ya Sahara ilishindwa kabisa kuendelea hasa kwa kuibuka kwa Biashara ya Pembetatu.
Utumwa uliochochewa na biashara utumwa
Biashara pia ilichochea (kufanya watu wapende biashara ya kuuza wenzao) vilivyo huko Afrika hasa katika upande wa Afrika Magharibi. Viongozi wengi wa Kiafrika walijihusisha vilivyo katika kununua na kuuza watumwa katika kanda hiyo.
Kuanguka kwa baadhi ya falme/dola
Biashara ya Pembetatu ilipelekea kuanguka kwa baadhi ya falme/dola huko Afrika Magharibi hasa zile ambazo zilitegemea kuuza bidhaa na si watumwa kwa Wazungu. Baadhi ya hizo dola ni pamoja na [[Dola la Ghana], Dola la Mali na Dola la Songhai na mengine mengi.
Kuibuka kwa baadhi ya baadhi ya madola
Biashara ilipelekea kukua kwa baadhi ya madola hasa yale yaliyokuwa yanategemea kuuza na kununua watumwa kama vile Tokolar, Ife, [[Dahomey[[ na kadhalika.
Maendeleo duni
Kiujumla biashara ilichochea kufifisha maendeleo ya Afrika katika nyanya zote ikiwa kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kupatikana kwa jamii kubwa za Wanegro hasa Brazil na Marekani
Watumwa waliopelekwa Amerika na sehemu nyingine walizaliana wenyewe kwa wenyewe au wanawake wao walipata mimba kwa Wazungu au wengineo. Ndiyo asili ya makundi makubwa ya watu wenye asili ya Afrika katika nchi kama Brazil, Marekani n.k. Hasa katika visiwa vingi vya Karibi, wakazi wengi leo wana asili hiyo.
Tazama pia
- Biashara ya ng'ambo ya Sahara
- Biashara ya masafa marefu ya Afrika Mashariki
- Biashara ya utumwa
- Mkutano wa Berlin wa 1885
- Historia ya Afrika
Viungo vya Nje
- Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki habari bila mipaka
- Biashara ya utumwa kupitia Atlantiki kwa watoto
- The Transatlantic Slave Trade Database, a portal to data concerning the history of the triangular trade of transatlantic slave trade voyages.
- Report of the Brown University Steering Committee on Slavery and Justice